Header Ads

Alichokisema Masau Bwire juu ya Simba SC kuelekea mechi yao

 

Watanzania kwa umoja wetu, tuombe kwa ajili ya Simba SC.....


Anaandika Masau Kuliga Bwire

Jioni leo, December 5, 2021, timu pekee ya Tanzania, Simba SC, inashuka uwanjani, ugenini, nchini Zambia, kucheza mchezo wa marudiano wa mashindano ya kombe la Shirikisho barani Afrika, dhidi ya Red Arrows ya huko.

Katika mchezo wa awali, uliochezwa nchini, kwenye uwanja wa Mkapa, wawakilishi wetu hao, Simba SC, waliibuka na ushindi mnono, bao 3-0.

Hatua hii ni ya mtoano, kwa hiyo, mshindi atakayemzidi mwingine, atasonga mbele hatua ya makundi, na atakayeziwa kwa pointi au mabao, atakuwa ameondolewa katika mashindano hayo.

Kwa matokeo ya mchezo wa awali, 3-0, mchezo wa leo, ili Watanzania na timu yetu ya Simba SC tuweze kusonga mbele, inahitajika sare ya aina yoyote, au isivyo bahati tukafungwa, zisizidi bao 2-0, hapo Watanzania tutakuwa tumeibuka kidedea na timu yetu ya Simba SC. 

Pamoja kwamba, Simba SC inayo nafasi kubwa sana ya kusonga mbele katika mashindano hayo,, ikibebwa na ubora na uimara wa kikosi chake, lakini pia matokeo mazuri ya mchezo wa awali, bado juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha inashinda, inatoa sare, na isifungwe zaidi ya bao 2-0.

Sina shaka na wachezaji wa timu hiyo ya Watanzania, Simba SC, wenye uzoefu mkubwa na hodari kwa mashindano makubwa ya Kimataifa, kubwa ninaloliomba kwa Watanzania wote, Wazalendo, wenye uchungu na maendeleo ya soka ndani ya nchi yetu, ni kuiombea dua njema, ishinde, na ifuzu kuendelea katika hatua nyingine ya makundi.

Tuweke kando tofauti zetu za kishabiki na kimapenzi tulizonazo katika ligi yetu ya ndani, tuungane Watanzania, tuwe wamoja, tuishabikie, tuishangilie na kuiombea ushindi, Simba SC, timu ya Tanzania inayotuwakilisha Watanzania katika mashindano hayo ya kimataifa.

Leo, kwenye vibanda umiza, niwasihi Watanzania wote, mosi, mavazi yetu yawe ya rangi nyeupe na nyekundu, yale mengine, yakiwemo ya njano na kijani tuyapumzishe, pili, muda wote wa mchezo tuiombee Simba SC, kila mmoja kwa imani yake ili ishinde, kwa kufanya hivyo, tutakuwa tumeutendea haki uraia wetu ndani ya nchi yetu, inayosifiwa na mataifa mengine kwa upendo, umoja, ushirikiano na mshikamano wetu.

Sisi ni Watanzania, Simba SC ni ya Tanzania na Watanzania ambao ndio sisi, tuiombee timu hii ya Watanzania, ishinde leo ili, Tanzania yetu, iendelee kusifika kimataifa kwa ubora wa soka.

Mungu ibariki Tanzania, 

Mungu ibariki Simba SC, 

Kwa uweza na maombi yetu, ushindi upatikane.

Masau Kuliga Bwire - Mzalendo.

Leave a Comment

No comments: